7: Kuzuia Magonjwa ya Figo

Tahadhari kwa mtu mwenye afya

Magonjwa ya figo huua kimya kimya. Yanaweza kusababisha kuendelea kwa kupotea kwa kazi ya figo na kuelekea kwa hitilafu ya figo na hatimae kuhitaji dayalisisi au kubadilisha kwa figo ili kudumisha maisha. Kwa sababu ya gharama kubwa na shida za kupatikana katika nchi zinazoendelea asili mia 5-10% ya wagonjwa wa hitilafu ya figo hupata matibabu kama dayalisisi na kubadilisha figo, wakati waliobaki hufa bila kupata tiba. Ugonjwa sugu wa figo ni tatizo kubwa sana na hauna tiba, kwa hiyo kinga ndio njia pekee. Ugunduzi na matibabu ya mapema huweza kuzuia hali ya ugonjwa sugu wa figo kuwa mbaya sana, na huweza kuzuia au kuchelewesha hata haja ya dayalisisi au kubadilisha/ kupandikizwa figo.

Ni vipi tunaweza kuzuia magonjwa ya figo?

Usipuuze figo zako. Mambo muhimu kuhusu kinga na utunzaji wa figo lenye ugonjwa wa figo yamejadiliwa katika sehemu mbili:

  1. Tahadhari kwa mtu mwenye afya.
  2. Tahadhari kwa mtu mwenye ugonjwa wa figo.

Tahadhari kwa mtu mwenye afya

Njia saba zinazofaa za kuweka figo kuwa zenye afya ni :

1. Kuwa mtu mwenye afya na mwenye kufanya mazoezi (Be fit and active)
Mazoezi ya kila mara na shughuli za kimwili za kila siku hudumisha msukumo wa kawaida wa damu na hudhibiti kisukari. Shughuli za kimwili huondoa hatari ya kisukari, na msukumo wa juu wa damu hivyo basi kupunguza hatari ya ugonjwa sugu wa figo.

2. Lishe bora
Kula lishe yenye afya, matunda na mboga mboga. Punguza ulaji wa vyakula vilivyosagwa, sukari , mafuta na nyama, chumvi kidogo hasa baada ya umri wa miaka 40 itasaidia kuzuia msukumo wa juu wa damu na kuwepo kwa mawe ya figo.

3. Chunga uzito wako
Dumisha uzito wako na lishe bora na mazoezi stahiki. Hii inaweza kuzuia kisukari, magonjwa ya moyo, magonjwa sugu ya figo na hali nyingine zinazohusishwa na ugonjwa sugu wa figo.

4. Acha uvutaji wa tumbaku na matumizi ya mazao ya tumbaku
Uvutaji wa tumbaku na matumizi mengine ya tumbaku yanaweza kusababisha atherosclerosis. Hii inaweza kupunguza mtiririko wa damu hadi kwenye figo na hivyo kupunguza uwezo wa figo kufanya kazi vyema.

5. Jihadhari na OTCs
Jihadhari na usizidishe matumizi ya dawa za kupunguza /kutuliza maumivu zinazonunuliwa bila karatasi ya Daktari (Prescription) kwenye kaunta. Dawa za kawaida kama non-steroidal anti-inflammatory kama ibuprofen zinajulikana kusababiaha uharibifu wa figo na hitilafu ya figo, zikitumiwa mara kwa mara. Pata ushauri wa daktari jinsi ya kudhibiti maumivu yako bila kuhatarisha figo zako.

6. Kunywa maji mengi
Unywaji wa maji ya kutosha ( Kiasi cha lita 3 kila siku ) husaidia kuzimua mkojo, kutoa uchafu wote wa sumu kutoka mwilini na kuzuia mawe kwenye figo.

7. Uchunguzi wa figo wa kila mwaka
Magonjwa ya figo huwa magonjwa yanayoingia mwilini kimya kimya na hayatoi dalili zozote hadi yafikie hatua ya kuimarika. Mbinu sahihi na bora lakini inayotumika kwa nadra sana ni uchunguzi wa mara kwa mara. Utambuzi wa mapema na kuzuia magonjwa ya figo inaweza kufanyika tu kwa uchunguzi wa kila mwaka. Watu walio kwenye hatari zaidi, kwa mfano wenye kisukari, unene kupita kiasi au walio na historia ya familia ya magonjwa haya ya figo ni vema wakafanya uchunguzi wa kila mwaka wa afya na hasa figo.

Ukipenda figo zako (Na hii ni muhimu zaidi kwako wewe mwenyewe) usisahau kupata uchunguzi wa mara kwa mara na hasa baada ya umri wa miaka 40. Njia rahisi ya ugunduzi wa mapema wa ugonjwa wa figo ni upimaji wa msukumo wa damu kila mwaka, upimaji wa mkojo na upimaji wa kreatinini kwenye damu.

Tahadhari Kwa Wagonjwa Wa Figo

Tahadhari Kwa Wagonjwa Wa Figo

1. Uhamasishaji kuhusu magonjwa ya figo na utambuzi wa mapema
Kuwa macho na makini ili utambue dalili za ugonjwa wa figo. Dalili za kawaida ni kuvimba kwa uso na miguu, kukosa hamu ya chakula, homa, kutapika, udhalifu, kukojoa kila mara, damu kwenye mkojo au kuwepo kwa protini kwenye mkojo. Wakati wa matatizo kama hayo, inashauriwa kupata ushauri wa daktari ili upate upimaji wa figo.

2. Tahadhari za kisukari
Kwa kila mgonjwa wa kisukari, tahadhari za kuzuia ugonjwa wa figo ni muhimu kwa sababu kisukari ndio sababu kuu ya ugonjwa sugu wa figo(CKD) na hitilafu ya figo kote duniani. Takriban asili mia 45% ya wagonjwa wapya wa hatua ya mwisho ya ugonjwa wa figo hutokana na kisukari. Kwa utambuzi wa mapema wa ugonjwa wa figo utokanao na kisukari njia rahisi na sahihi ni upimaji wa mkojo ili kubaini kuwepo kwa protini na msukumo wa damu kwa kila miezi mitatu. Upimaji bora zaidi wa utambuzi wa mapema kwenye kisukari ni upimaji wa maikroalbuminuria (MA) kwenye mkojo, ambao unafaa kufanywa kila mwaka. Aidha pima kreatinini ya damu ( na e GFR) ili kuchunguza kazi ya figo angalau mara moja kila mwaka.

Msukumo wa juu wa damu, kuwepo kwa protini kwenye mkojo, kuvimba, upungufu wa sukari kwenye damu wa kila mara na kuonekana kwa dalili za kisukari kwenye jicho(diabetic retinopathy) ni vidokezo muhimu kwa figo kuhusishwa na kisukari. Jihadhari na ishara hizi hatari na upate ushauri wa daktari wako mapema.

Ili kujikinga na ugonjwa wa kisukari ya figo, wagonjwa wote wa kisukari wana wajibu wa kudhibiti kwa uangalifu sana kisukari, kudumisha msukumo wa damu uwe chini ya 130/80 mm ya Hg(ace. Inhibitor au ARB ni dawa zinazopendekezwa kwa kudhibiti msukumo wa juu wa damu) punguza kiwango cha protini kwa lishe na dhibiti mafuta.

3. Tahadhari kwa wagonjwa wenye msukumo wa juu wa damu
Msukumo wa juu wa damu ndio chanzo cha pili muhimu cha ugonjwa sugu wa figo ambacho kinazuilika. Na kwa kuwa wagonjwa wengi wenye tatizo la msukumo wa damu hawaonyeshi dalili zozote, wengi husitisha matibabu kwa muda na wachache husitisha matibabu kabisa kwa kuwa wao huhisi vyema bila dawa. Lakini hii ni hatari. Msukomo usiodhibitiwa kwa muda mrefu huweza kusababisha shida na hatari kama ugonjwa sugu wa figo , moyo kusimama ghafla na kupooza.

Ili kukinga ugonjwa wa figo, wagonjwa wote wa msukumo wa juu wa damu , wanatakiwa kunywa dawa zao kila mara/kila siku, kuchunguzwa msukumo wa damu na kuwa na lishe/mlo bora na kuepuka mlo wenye chumvi. Madhumuni yawe kuweka presha /msukumo wa damu kuwa chini ya 130/80mm ya Hg. Ili kutambuwa mapema uharibifu wa figo wagonjwa wote wenye msukumo wa damu wachunguzwe mkojo na kreatinini ya damu kila mwaka.

4. Tahadhari kwa ugonjwa sugu wa figo
Ugonjwa sugu wa figo hautibiki. Lakini utambuzi wa mapema na udhibiti wa mlo,na kufuatia maelekezo ya matibabu bora itapunguza mwendelezo wa ugonjwa na kuchelewesha hatua ya matumizi ya dayalisisi au kubadilisha figo.

Udhibiti thabiti wa msukumo wa juu wa damu ni hatua muhimu ya kuzuia kwendelea kwa ugonjwa sugu wa figo. Inapendekezwa sana kuweka msukumo wa damu kuwa 130/80 mm Hg au chini. Njia nzuri ya kuthibiti msukumo wa damu ni kupima mara kwa mara hata nyumbani na kuandika sehemu ili kumsaidia daktari wako kuamua kiasi gani cha dawa akupe.

Kwa wagonjwa wenye CKD, vidokezo kama msukumo wa chini wa damu (hypotension),kupungua maji mwilini (dehydration), kuwa na kizuizi kwenye mfumo wa mkojo (obstruction), maambukizi kwenye damu (sepsis), dawa zinazoumiza figo……nk lazima zitambuliwe. Kuchukuliwa hatua za haraka katika vidokezo hivi kunaweza kuleta nafuu kwa figo hata katika hali ya CKD.

5. Utambuzi na matibabu ya ugonjwa wa polisistiki ya figo (PKD)
Ugonjwa huu (ADPKD) ni hitilafu ya figo ambayo hurithiwa na hujumuisha asili mia 6-8 % ya wagonjwa walio katika dayalisisi. Mtu mzima ambaye ana historia ya ugonjwa huu wa figo yuko katika hatari kubwa sana na anastahili kuchunguzwa mapema na picha ya ultrasound ili ugonjwa ugundulike mapema. PKD haina tiba, lakini hatua kama kudhibiti msukumo wa juu wa damu, matibabu ya maambukizi ya mfumo wa mkojo, kuthibiti lishe na usaidizi wa matibabu(supportive treatment) husaidia kudhibiti dalili, kuzuia matatizo makubwa (complications), na kupunguza kasi ya utendaji kazi wa figo.

6. Utambuzi na matibabu ya mapema ya maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa watoto
Maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI) lazima uhisiwe wakati mtoto anapata baridi isiyoelezeka, kukojoa kila mara, kuchomwa wakati wa kukojoa, ukosefu wa hamu ya kula na ongezeko mbaya wa uzito.

Ni muhimu kukumbuka kuwa kila maambukizi ya mfumo wa mkojo yanapotokea (UTI), hasa yenye homa husababisha uharibifu wa figo hasa isipotambuliwa, tiba ikiwa imechelewa au kutomaliza matibabu. Uharibifu unaoweza kutokea ni pamoja na figo kuwa na makovu, figo kutokukua, msukumo wa juu wa damu, na figo kushindwa kufanya kazi baadae katika maisha. Kwa sababu hii maambukizi haya kwa watoto hayahitaji tu utambuzi wa mapema au matibabu ya haraka, bali pia tathmini makini ili kubaini vihashiria vingine, hatari au athari nyingine. Vesicoureteral reflux (VUR) ndiyo chanzo kikuu cha maambukizi haya na huleta karibu asili mia 50% ya jumla ya maambukizi yote wakati wa utoto. Ufuatiliaji ni muhimu sana kwa watoto waliopatwa na UTI.

7. Maambukizi ya mfumo wa mkojo unaojirudia rudia kwa watu wazima
Wagonjwa wote wenye maambukizi ya mfumo wa mkojo yenye kujirudia rudia wanahitaji kujua sababu zake. Baadhi ya sababu ni uzibaji wa mkondo wa mkojo, tiba isiyo kamili, ugonjwa wa mawe n.k) Matatizo haya yasipotibiwa vizuri huweza kuharibu figo. Kwa hiyo utambuzi wa mapema na matibabu ya vyanzo vya tatizo kujirudia rudia ni muhimu.

8. Matibabu sahihi ya ugonjwa wa mawe Na kuvimba kwa tezi dume (BPH)
Wagonjwa wengi wanaouguza ugonjwa wa mawe hawana dalili zozote kwa hivyo wanakosa kugundua ugonjwa na kukosa utambuzi na matibabu yake kwa wakati/ mapema. Wanaume wengi wazee walio na tezi dume (BPH) hawatambui dalili zake kwa muda mrefu. Tatizo la mawe na tezi dume kama hayakutibiwa mapema na kwa wakati huweza kuleta uharibifu kwenye figo. Ufuatiliaji sahihi na tiba ya wakati husaidia sana kulinda figo.

9. Usipuuze msukumo wa damu katika umri mdogo
Msukumo wa damu katika umri mdogo si kitu cha kawaida na kwa hiyo huhitaji uchunguzi kamili wa chanzo chake. Magonjwa ya figo ndiyo yanaweza kusababisha msukumo wa juu wa damu kwa vijana. Kwa kila kijana mwenye msukumo wa juu wa damu anahitaji kufanyiwa utambuzi wa magonjwa ya figo na matibabu sahihi ili kulinda figo ya mgonjwa huyu.

10. Matibabu ya mapema ya hitilafu kali ya figo
Vyanzo muhimu vya hitilafu kali ya figo ni kushuka ghafla kwa utendaji wa figo. Hii utokea katika matatizo yafuatayo: kuhara, kutapika, malaria (hasa aina ya falsiparumu), maaambukizo katika damu (sepsis), madawa mengine (ACE inhibitor, NSAID’s) n.k matibabu ya mapema na bora ya vyanzo hivi huweza kuzuia hitilafu ya figo.

11. Tahadhari kuhusu matumizi ya dawa
Kuwa mwangalifu. Dawa nyingi zinazonunuliwa dukani hasa za kutuliza maumivu, zina hatari ya kusababisha uharibifu wa figo hasa kwa wazee. Dawa kama hizo zinatangazwa bila kueleza hatari zinazobainishwa kwa wanunuzi. Acha matumizi ya dawa hizi kwa mauimivu ya kichwa na mwili. Pia usijitibu mwenyewe na dawa zisizofaa. Ni vyema kupata maelezo na maelekezo ya daktari kuhusu matumizi salama ya dawa. Ni vibaya kuamini kuwa dawa zote za asili na badala (Ayurvedic medicines, Chinese herbs….nk) pamoja na virutubisho vya vyakula (dietary supplements) si hatari.

Vyuma vizito vilivyo kwenye dawa za Ayurvedic vinaweza kusababisha uharibifu wa figo.

12. Tahadhari kwa figo moja
Watu walio na figo moja huishi maisha sawa na yenye afya. Kwa kuwa watu hawa hawana figo nyingine, tahadhari lazima zichukuliwe. Mgonjwa adhibiti msukumo wa damu, anywe maji mengi, awe na lishe bora, apunguze /adhibiti ulaji wa chumvi, asile vyakula vyenye viwango vya juu vya protini, na kwa namna yoyote ile azuie jeraha la hiyo figo moja. Tahadhari muhimu zaidi ni uchunguzi wa kiafya wa mara kwa mara. Inafaa amuone daktari mara moja kwa mwaka ili kuchunguza kazi ya figo kwa kuangalia msukumo wa damu, upimaji wa mkojo na damu, pia upimaaji wa ultra sonogramu ,iwapo inahitajika.