16: Ugonjwa wa Figo wa Polisitiki (Polycystic)

Ugonjwa wa figo wa uvimbe uliojaa maji (polycystic kidney disease - PKD).

Ugonjwa huu ndio ugonjwa wa figo wa kawaida sana ambao hurithiwa.Ni ugonjwa wa figo kuvimba vibofu vingi vingi.Ndio nambari ya nne kati ya vyanzo vinavyosababisha ugonjwa sugu wa figo.Viungo vingine vya mwili vinavyoweza kupata vibofu hivi ni ini, ubongo, matumbo, kongosho, ovari na wengu.

Matukio ya vimbe za figo

Ugonjwa wa vimbe za figo hupatikana kwa watu wa asili zote, wake kwa waume na humpata mtu mmoja kwa kila watu elfu duniani kote. karibu asilimia tano ya wagonjwa wote wanaohitaji dayalisisi au kupatiwa figo huwa na vimbe za figo.(PKD)

Figo huathirika vipi na vimbe?(PKD)

 • Figo zote mbili huvimba vibofu vingi vingi vilivyojaa maji.
 • Vibofu hivi hutofautiana kwa ukubwa kuanzia vidogo kama sindano hadi vyenye upana wa hata sentimita kumi au zaidi.
 • Kadri muda unavyo endelea vibofu huendelea kukua na polepole huendelea kufinya na kuharibu figo.
 • Uharibifu huu husababisha shinikizo la damu, kuwepo kwa protini kwenye mkojo na kazi za figo kudhoofika na mwishowe ugonjwa sugu wa figo hujitokeza.
 • Shida hii ikiendelea kwa muda mrefu figo huzidi kudhoofika (hadi ESKD) na huenda mgonjwa akahitaji dayalisisi au figo nyingine.

Dalili

Dalili za ugonjwa wa figo kuvimba vibofu (PKD)

Watu wengi huishi miaka mingi bila dalili zozote.wengi huonyesha dalili baada ya umri wa miaka thelathini au arobaini. Dalili za kawaida ni:

 • Shinikizo la damu.
 • Maumivu ya mgongo (upande mmoja au pande zote), mbavu , au tumbo kuvimba.
 • Kuhisi uvimbe mkubwa tumboni.
 • Damu au protini kwenye mkojo.
 • Maambukizi ya njia ya mkojo ya mara kwa mara na mawe ya figo.
 • Dalili za ugonjwa sugu wa figo jinsi figo zinavyoendelea kudhoofika.
 • Dalili zinazotokana na vimbe katika sehemu zingine za mwili kama ubongo, ini au kwenye matumbonk.
 • Matatizo ambayo mgonjwa anaweza kupata ni kama ubongo kuvimba (brain aneurysm), henia kwenye tumbo,ini kupata maambukizi, pochi sehemu ya mwisho ya utumbo (colon) na magonjwa ya moyo kwenye valve. Karibu asilimia kumi ya wagonjwa huvimba mishipa ya ubongo (aneurysm).Hali hii humfanya mtu aumwe na kichwa na kuwa katika hatari ya mshipa kupasuka na kusababisha kupooza na hata kifo.

Je, ni lazima figo zinazovimba vibofu zishindwe kufanya kazi?

  Hapana .Sio kila mgonjwa hupata ugonjwa wa kufeli kwa figo. Takriban asilimia hamsini hupata ugonjwa wa figo kufeli wakiwa na umri wa sitini,na kama asilimia sitini hupata wakiwa na miaka sabini.Wanaume sana sana ndio hufeli figo pia wanaopata vimbe hizi za figo wakiwa na umri mdogo,walio na shinikizo la damu na protini au damu kwenye mkojo pia huwa na figo kubwa.
PKD ni ugonjwa wa figo wa kurithi unaojulikana sana na ni wan ne kwa kuleta CKD.

Utambuzi

Utambuzi wa vimbe za figo.(PKD)

Vipimo vinavyotumika ni:

 • Ultrasound ya figo: Kipimo hiki hutumika sana kwa kuwa kinaaminika, rahisi, salama,hakina maumivu na kina gharama kidogo.
 • Picha za CT au MRI - Vipimo hivi huwa sahihi zaidi ingawaje ni ghali.Huweza kuonyesha vivimbe vidogovidogo kabisa ambavyo haviwezi kuonekana kwa picha ya ultrasound.
 • Familia kuchunguzwa; Vimbe za figo huwa ni ugonjwa unaorithiwa kwa wazazi na kila mtoto ana hatari ya kupata ugonjwa huu kwa kiasi cha 50:50. Kwa hiyo, familia ya mgonjwa inafaa kupimwa mara moja.
 • Vipimo vya madhara ya vimbe kwenye figo: Mkojo hupimwa ili kuchunguza uwepo wa damu au protini kwenye damu. Kreatinini hupimwa ili kuchunguza na kufuatilia kazi ya figo.
 • Kutambuliwa ugonjwa huu kwa bahati: Vimbe za figo zinaweza kuonekana kwa bahati mtu anapopimwa kawaida au anachunguzwa kwa picha za ultrasound kwa sababu nyingine.
 • Kuchunguza kuzingatia uhusiano wa kijeni au kidamu (gene tests). kipimo hiki hutumiwa kuchunguza ni nani kwenye familia ana jeni za ugonjwa huu.kipimo hiki kinafaa kutumiwa iwapo vipimo vya picha havionyeshi chochote.Kipimo huwa kinapatikana katika vituo vichache na ni ghali sana.

Kwa familia ni nani afaa kupimwa kuchunguza vimbe za figo?

Ndugu na watoto wa mgonjwa wanafaa kupimwa. Pia ndugu wa wazazi wa mgonjwa.

Je, ni watoto wote wa mgonjwa wako katika hatari ya kupata vimbe za figo?

La,vimbe za figo ni ugonjwa unaorithiwa iwapo baba au mama anao,watoto wana uwezekano wa asilimia hamsini ya kuupata pia.

Maumivu ya mbavu na mgongo au damu kwenye mkojo katika umri wa arobaini huwa dalili ya vimbe kwenye figo.

Kuzuia

Kuzuia vimbe za figo
Kupunguza vimbe za figo:
Familia yote kupimwa mapema kabla ya ugonjwa kuanza kuna faida nyingi. Ugonjwa unapojulikana mapema, huweza kutibiwa vyema zaidi. Kutambua na kutibu shinikizo la damu huzuia kuendelea au kuzidi kwa figo kudhoofika.Kubadili mienendo na vyakula kwa wagonjwa wa vimbe za figo hukinga figo zao na pia moyo.Ubaya wa kupimwa ni kwamba mtu anaweza kushikwa na wasiwasi ilhali hana dalili zozote na hata hahitaji matibabu yoyote.

Kwa nini ni vigumu kupunguza matukio ya vimbe za figo?

Ugonjwa huu kwa kawaida hutambuliwa katika umri wa miaka arobaini au zaidi.Wengi huwa na watoto kabla ya umri huu na hivyo vigumu kuzuia kupitia kwa vizazi.

PKD ni ugonjwa wa figo wa kurithi, kwa hiyo ni vyema kuwapima watu wazima wote wa familia hiyo ili kuona kama yeyote ana PKD.

Matibabu

Matibabu ya vimbe za figo
 • Vimbe za figo hauna tiba ya kuponesha lakini huhitaji matibabu ili kulinda figo na kuzuia kukua kwa ugonjwa sugu wa figo hadi kufikia kipindi chake cha mwisho (ESKD)hivyo nia iwe kuendeleza uhai.
 • Kuzuia dalili na matatizo yanayoweza kuambatana na hali hii (complications).
Mambo muhimu katika matibabu ya vimbe za figo:
 • Mgonjwa huwa hana dalili zozote kwa miaka mingi baada ya ugonjwa kutambulika,na hivyo hahitaji matibabu yoyote. Wagonjwa kama hawa huhitaji kuangaliwa na daktari mara kwa mara.
 • Kuhakikisha kuwa shinikizo la damu limezuiliwa na hivyo kupunguza kasi ya ugonjwa sugu wa figo.
 • Kuzuia maumivu kwa dawa ambazo hazidhuru figo kama vile aspirin au acetaminophen . Inawezekana kukawa na maumivu ya mara kwa mara au hata wakati wote. Hii ni kwa sababu vimbe zinakua.
 • Kutibu mara moja maambukizi ya njia ya mkojo kwa kutumia dawa za antibayotiki zinazofaa.
 • Kutibu mawe ya figo mapema.
 • Kunywa vinywaji kwa wingi kama mgonjwa hajavimba.Hii huzuia maambukizi ya njia ya mkojo na mawe ya figo.
 • Matibabu bora ya ugonjwa sugu wa figo kama ulivyoelezwa katika sura ya 10-14.
 • Kwa wagonjwa wachache vibofu hupasuliwa ili kuvitoa maji kwa sababu ya maumivu, kutokwa na damu,maambukizi au njia ya mkojo kufunga.
Matibabu hulenga kupunguza kuendelea kwa ugonjwa sugu wa figo, kutibu maambukizi ya figo, mawe ya figo na maumivu tumboni.
Je, mgonjwa wa vimbe za figo anafaa kumwona daktari lini?

Mgonjwa anafaa kumwona daktari mara moja iwapo:

 • Ana homa,maumivu ya tumboni ya ghafla au mkojo mwekundu.
 • Maumivu makali au yanayo jirudia rudia ya kichwa.
 • Kujeruhiwa figo au figo kuongezeka ukubwa.
 • Maumivu ya kifua, kukosa hamu ya chakula, kutapika sana, misuli kukosa nguvu,kuchanganyikiwa , kusinzia au kuzimia.

Mgonjwa ambaye hana dalili anaweza kukaa kwa miaka mingi bila ya kuhitaji matibabu.