Mfumo  wa mkojo huundwa na figo, njia ya mkojo inayotoka kwenye figo hadi kwenye kibofu(yureta),kibofu cha mkojo na njia ya mkojo inayotoka kwenye kibofu hadi nje ya mwili(yurethra).Maambukizi ya bacteria  huweza  kuathiri sehemu yoyote ya mfumo huu. Maambukizi ya mfumo wa mkojo ni ya pili ukiangalia maambukizi yote ya mwili.
Dalili za maambukizi  ya  mfumo  wa  mkojo  ni zipi? 
Dalili  hutofautiana  kulingana na ukali wa maambukizi,umri na sehemu iliyoathirika.
Dalili zinazojitokeza mara nyingi pakiwa na maambukizi (UTI): 
    - Uchungu au kuwashwa unapokojoa.
 
    - Kuhisi kukojoa mara nyingi.
 
    - Homa na uchovu .
 
    - Mkojo wenye harufu mbaya na si safi  (cloudy).
 
Dalili zinazotokana  na maambukizi ya  kibofu 
    - Maumivu katika upande wa chini wa tumbo.
 
    - Kukojoa mkojo kidogo , wenye maumivu na mara nyingi.
 
    - Dalili za homa kidogo. Bila maumivu ya mbavu.
 
    - Damu kwenye mkojo.
 
Dalili  zinazotokana na maambukizi ya upande wa juu wa njia ya mkojo 
    - Maumivu  ya upande wa juu wa mgongo na mbavu.
 
    - Kuwa na homa na kuhisi kibaridi. Kichefuchefu, kutapika, uchovu na kujihisi mgonjwa kwa ujumla.
 
    - Kuchanganyikiwa  kwa  wazee.
 
Maambukizi haya ni hatari sana yasipotibiwa vyema na haraka. Aidha yanaweza  hata kuhatarisha maisha.
Kuwashwa na kukojoa mara nyingi ni dalili za maambukizi ya sehemu za mfumo wa mkojo.
                         
                    
                       
                            
                            Nini   kinachosababisha maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya mkojo? 
1. Kuziba kwa  njia ya mkojo.
2. Maumbile ya kike    Kwa sababu njia ya yurethra ya wanawake ni fupi kuliko ya wanaume,basi huwezekano wa  kupata maambukizi ni  mkubwa  zaidi  kuliko  wanaume.
3. Maingiliano/ Kujamiiana:   Wanawake wanaoshiriki tendo la ndoa huweza kupata maambukizi  mengi zaidi kuliko wenzao wasioshiriki tendo hilo.
4. Mawe  Mawe kwenye figo,   njia ya kuelekea kwenye  kibofu cha mkojo (ureta) au ndani ya kibofu chenyewe  yanaweza kuzuia mtiririko wa mkojo na hivyo kusababisha maambukizi.
5. Mpira wa katheta   Watu  waliowekewa   katheta wana uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi kirahisi.
6. Kasoro za kimaumbile   Watoto wenye kasoro  za kimaumbile kama mkojo  kurudi nyuma  kama kwenye kibofu na hivyo kwenda kwenye yureta ( vesicoureteral reflux)  au kama  njia ya yurethra valve inafungukia nyuma, hupata maambukizi  kwa urahisi sana.
7. Kuongezeka ukubwa wa tezi dume     Wanaume walio na umri wa miaka zaidi ya sitini wanaweza kupata maambukizi  kwa sababu ya kukua kwa tezi dume.
8. Kinga ya mwili iliyodhoofika     Wagonjwa wa kisukari,UKIMWI au saratani.
9. Sababu nyingine:       kama  njia  za  yureta  na  yurethra  kuwa nyembamba,tibi  (TB)  kwenye  njia  ya mkojo,  neurogenic bladder,diverticulumnk.
Kuziba  njia ya mkojo ni sababu kuu ya maambukizi ya njia ya mkojo.
                         
                    
                       
                            
                            Je,maambukizi  ya  mara kwa mara hudhuru figo? 
Maambukizi  ya mara kwa mara kwa watu wazima hayawezi kudhuru figo .  Kitu muhimu cha kuangalia ni hali iliyosababisha maambukizi hayo, kama  mawe,   kuziba au njia kuwa nyembamba, tibii ya mfumo wa mkojo  havijatibiwa ipasavyo.
kwa upande mwingine,maambukizi kwa watoto yasipotibiwa kwa haraka na kwa njia ifaayo,figo zao changa zinaweza kuharibika kabisa. Madhara  haya yanaweza kufanya uwezo wa figo wa kufanya kazi upungue na mtoto kupata shinikizo la damu.  Kwa hiyo maambukizi haya ni hatari zaidi kwa watoto kuliko watu wazima.
Utambuzi wa maambukizi ya sehemu za mfumo wa mkojo 
Uchunguzi  hufanywa ili kutambua ugonjwa na kujua ukali wake.Kwa mtu ambaye hupata maambukizi haya mara kwa mara au  yenye matatizo mengi,vipimo tofauti hufanywa ili kujua chanzo cha ugonjwa na hatari zilizopo zinazomfanya kupata tatizo hili mara kwa mara.
1. Uchunguzi wa msingi wa maambukizi ya mfumo wa mkojo 
1 Kuchunguza mkojo 
Uchunguzi ambao ni hupendekezwa sana ni  kupima mkojo wa kwanza wa asubuhi . Mkojo kama una chembechembe nyeupe za damu nyingi huashiria maambukizi. Hata hivyo,kutopatikana kwa chembechembe hizi huwa haimaanishi hakuna maambukizi.Vijiti vyenye kemikali ambavyo hubadilika rangi vikiwekwa kwenye mkojo pia huweza kutumiwa nyumbani na hata ofisini.Jinsi rangi inavyobadilika ndivyo huashiria wingi wa bakteria kwenye mkojo.  Vijiti hivi havipatikani kwa urahisi katika nchi nyingine kwa mfano India.
Maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa kawaida hauleti uharibifu kwenye figo na hasa kama hakuna sehemu yoyote iliyoziba kupitisha mkojo.
                         
                    
                       
                            
                            2. Ukuzaji wa bacteria ili kuzichunguza 
Uchunguzi huu ndio bora zaidi na unafaa kufanywa kabla ya kutumia dawa za antibayotiki.Hupendekezwa kwa maambukizi yenye matatizo mengi ,pia hufanywa kuthibitisha  kile ambacho daktari alikuwa amewazia.
Ukuzaji huu huwa kwa saa 48-72,wakati huu mrefu wa kungoja ndilo tatizo kubwa la uchunguzi huu. Jinsi bakteria   Wanavyokua kipimo hiki hutumiwa kutathmini uwepo na ukali wa maambukizi  pia aina ya viumbehai vilivyosababisha maambukizi.Aina ya bacteria iliyosababisha maambukizi hujulikana na hivyo dawa za antibayotiki zinazotakiwa kutumika huamuliwa.
Ili kuzuia mkojo wa uchunguzi kuchafuka,mgonjwa hutakiwa asafishe sehemu za siri na kuchukua sampuli ya mkojo wa kati (mid stream) kwenye kichupa safi.  Vifuko vya katheta pia hutumiwa kupata sampuli ya mkojo. Njia nyingine ni kupata mkojo moja kwa moja toka kwenye kibofu kwa kutumia sindano.
3. Kupimwa damu 
Vipimo vya damu ambavyo huombwa mara nyingi ni pamoja na vile vya chembechembe nyekundu na nyeupe za damu, yurea kwenye damu, kiasi cha kreatinini,sukari ya damu na protini.
Kukuza  adudu  na  kuona wanasikiaje  dawa(culture  and  sensitivity)  ni  kipimo muhimu sana kwa utambuzi na kutibu mambukizi kwenye mfumo wa mkojo.
                         
                    
                       
                            
                            Uchunguzi ili kujua hali zingine za hatari zinazoambatana na maambukizi
Iwapo maambukizi hayaishi au yanarudi tena na tena, utafiti zaidi unahitajika kuchunguza iwapo kuna matatizo mengine,uchunguzi  huo huzingatie :
1. Picha za ultrasound na eksirei ya tumbo.
2. Picha za CT  na MRI  za tumbo.
3. Voiding cystourethrogram.
4. Intravenous urography.
5. Kupima ugonjwa wa tibii (TB) ya mkojo.
6. Kuangalia ndani ya kibofu cha mkojo kwa kutumia mashine inayoitwa cytoscope.
7. Kupimwa na daktari wa uzazi .(kama ni mwanamke).
8. Urodynamics.
9. Kupima damu ili kuotesha wadudu -  (blood cultures).
Kwa matibabu bora ya maambukizi ya njia ya mkojo ni muhimu kuchunguza chanzo cha matatizo anayoambatana na ugonjwa.
                         
                    
                       
                            
                            Kuzuia maambukizi  ya  mfumo wa mkojo 
    - Kunywa maji  mengi ,lita tatu hadi nne kila siku.  Maji huzimua mkojo na kusaidia kutoa bacteria kwenye kibofu na njia ya mkojo.
 
    - Kukojoa kila baada ya saa mbili au tatu,usihairishe kukojoa,kuweka mkojo kwa muda mrefu huwapa  bacteria nafasi ya kukua.
 
    - Kula vyakula vyenye vitamini  C ,kama vile matunda, ( ubuyu, machungwa…nk), mkojo wenye asidi hupunguza bacteria.
 
    - Zuia kufunga choo au tibu hali hii mara moja.
 
    - Wanawake na wasichana wajipanguse  kutoka mbele wakielekea nyuma na si nyuma hadi mbele  baada ya kujisaidia.
 
    - Kusafisha  sehemu za siri ,mbele na nyuma baada ya kufanya mapenzi,kojoa kabla na baada ya kufanya mapenzi na kunywa gilasi ya maji  baadaye.
 
    - Wanawake wanashauriwa kuvaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba ili kuruhusu hewa kuzunguka.Nguo za ndani za nailoni hazifai.
 
    - Maambukizi   yanayorudi tena na tena baada ya kufanya mapenzi yanaweza kuzuiwa kwa kutumia dozi moja tu ya dawa za antibayotiki.
 
Ni muhimu kunywa maji mengi ili kuzuia na kutibu maambukizi ya njia ya mkojo.
                         
                    
                       
                            
                            Matibabu ya maambukizi  ya mfumo wa mkojo Hatua za jumla 
Kunywa maji mengi.  Kama mtu ni mgonjwa sana ,ameishiwa na maji mwilini au hawezi kunywa maji kwa sababu ya kutapika,anahitaji kulazwa hospitalini na kuwekewa maji.
Kunywa dawa za kupunguza  maumivu na dalili ya homa.  Tumia vitambaa moto kujikanda hupunguza  maumivu. Usinywe  kahawa wala pombe, usivute sigara au kula vyakula vyenye viungo vikali.  Hivi vyote husumbua kibofu.  Zingatia hatua zote za kuzuia maambukizi.
Kutibu  maambukizi  ya sehemu ya chini  ya mfumo wa mkojo 
Kwa mwanamke wa umri mdogo,dawa za antibayotiki kwa siku tatu tu zinatosha.Madaktari wengine hupendelea kutoa dawa hizi kwa siku saba hadi kumi na nne. Wanaume  huitaji matibabu ya sku  7 hadi 14 ya antibiotiki. Dawa ambazo mara nyingi hutumiwa ni trimethoprim, cephalosporins,  nitrotuyantoin au  fluoroquinolones.
Matibabu  ya maambukizi makali ya  figo(Pyelonephritis) 
Wagonjwa wenye maambukizi makali huhitaji kulazwa hospitalini.Mkojo na damu hupimwa kabla ya kuanza matibabu ili kubaini chanzo na kuamua dawa zinazofaa.Wagonjwa hutibiwa kwa kuwekewa maji na dawa  za antibiotiki kupitia kwenye mshipa . Hii hufuatiwa na tembe za antibayotiki kwa siku kumi hadi kumi na nne. Ikiwa dawa zinazotolewa hazisaidii na mgonjwa anazidi kuwa na dalili za maambukizi na homa na kuonyesha dalili za  kudhoofika kwa figo,picha hupigwa. Mkojo hupimwa tena  ili kutadhmini  maendeleo ya matibabu.
Maambukizi ya mfumo wa mkojo ya mara kwa mara 
Kwa mgonjwa mwenye maambukizo yanayo jirudiarudia, ni  muhimu kutambua chanzo  kinachosababisha maambukizi hayo.  Kutegemea chanzo chake, matibabu ya dawa au upasuaji hupangwa.Wagonjwa kama hawa huhitaji kufuatiliwa,kuzingatia ushauri  wa kujitunza na dawa za antibayotiki kwa muda mrefu.
Mgonjwa mwenye maambukizi kwenye njia ya mkojo inafaa amwone daktari lini? 
    - Mkojo ukipungua au kupotea kabisa.
 
    - Homa kali, kutetemeka, maumivu ya mgongo, mkojo usio safi (cloudy) au  mwekundu.
 
    - Mgonjwa  anayetapika sana,  misuli kukosa nguvu na shinikizo la damu kuwa chini.
 
    - Watoto wote wenye maambukizi ya mfumo wa mkojo.
 
    - Wagonjwa wote wenye figo moja au/na historia ya kuwa na mawe.
 
    - Hakuna nafuu baada ya matibabu ya antibitiki kwa siku 2 hadi 3.
 
Homa kali kwa muda mrefu, homa ya baridi (chills), mkojo mchafu, kuunguza wakati wa kukojoa, hizi zote zinahitaji uchunguzi makini.