20: Uvimbe usio wa Saratani kwenye Tezi dume

Tatizo la tezi dume kupanuka

Tezi dume hupatikana kwa wanaume tu.Tezi hili likiongezeka kwa ukubwa yaani inapopanuka,hasa kwa wanaume wenye umri wa zaidi ya miaka sitini, hutatiza kukojoa.Ugonjwa huu unazidi kuongezeka duniani kwani watu wanaishi maisha marefu zaidi siku hizi.

Tezi dume ni nini na kazi yake ni nini?

Tezi dumeni kiungo kidogo na ni sehemu moja ya uzazi wa wanaume.Hupatikana chini ya kibofu na mbele ya mwanzo cha njia itoayo mkojo hupitia ndani ya tezi dume.Tezi dume ndiyo hutoa maji yabebayo mbegu (manii)ya mwanaume.

Tezi dume kupanuka

Kupanuka kwa tezi dume ni tatizo la kawaida ambalo halisababishwi na ugonjwa wa saratani(kansa).Huwa ni jambo la kawaida kwa karibu kila mwanaume mzee.Miaka inavyoenda,ndivyo tezi dume huzidi kuwa kubwa; na hufinya njia ya mkojo na kuziba mkojo.Hivyo mkojo hutoka polepole .

Ugonjwa wa kutanuka kwa tezi dume ni ugonjwa wa wanaume wazee.

Dalili za kupanuka kwa tezi dume

Dalili huonekana baada ya umri wa miaka ya hamsini . Karibu wanaume wote wenye umri wa sabini na themanini huwa na tatizo hili.Dalili huanza polepole na kuzidi jinsi miaka inavyoongezeka.Dalili hizi ni kama zifuatazo:

 • Kukojoa mara nyingi hasa nyakati za usiku.Hii ni dalili ya mapema sana.
 • Kulazimika, mara nyingi hasa nyakati za usiku, kutumia nguvu kuanzisha mkojo kutoka. Hata pale mgonjwa anahisi kibofu kimejaa. Hii ni dalili ya mapema sana.
 • Mkojo kutiririka polepole, hukatikakatika na hutumia nguvu kutoka.
 • Mkojo kushidwa kutoka hata wakati mtu anapohisi kukojoa.
 • Mkojo kuendelea kutoka kidogokidogo baada ya kukojoa, matone ya mkojo huendelea kutoka hata baada ya kukojoa hivyo nguo za ndani hulowa.
 • Kibofu hakiishi mkojo.

Matatizo ya tezi dume iliyotanuka

Tezi dume ikitanuka sana huleta matatizo mengi kwa wagonjwa wengine hali hii isipotibiwa. Matatizo hayo ni kama yafuatayo:

 • Mkojo kukosa kutoka kabisa
  Wagonjwa wenye tatizo hili lazima wawekewe katheta ili kumimina mkojo.
 • Madhara kwenye kibofu na figo
  Kwa sababu ya kibofu kuwa na mkojo wakati wote, ukuta na misuli yake hupanuka na mwishowe hudhoofika hivi kwamba haiwezi kuzuia mkojo.
 • Kwa sababu ya kibofu kujaa
  mkojo hurudi kwenye figo na mwishowe huharibu figo.
Ugonjwa wa tezi dume husababisha mkojo kutiririka polepole na mtu kukojoa mara nyingi hasa usiku.

 • Maambukizi na mawe
  Kwa sababu kibofu hakimimini mkojo wote kuna hatari kubwa ya maambukizi kwenye njia ya mkojo nakuwa na mawe kwenye kibofu.
 • Kumbuka
  Kutanuka kwa tezi dumehakusababishi ugonjwa wa saratani.
 • Utambuzi wa kupanuka kwa tezi dume
  Historia na dalili zikiashiria uwepo wa hali hii, basi uchunguzi ufuatao hufanywe.
 • Uchunguzi wa ukubwa wa tezi
  Uchunguzi huu hufanywa kwa kuingiza kidole chenye glavu nyuma hadi kwenye tezi dume. Daktari huweza kujua ukubwa na hali yake. Iwapo mtu ana ugonjwa huu tezi dume ni kubwa kuliko kawaida, laini na gumu yote pamoja. Iwapo tezi lina vifundo basi inaweza kuwa na kansa (saratani)au inaweza kuwa na kalsium.
 • Vipimo vya picha ya ultrasound na kiasi cha mkojo kwenye kibofu
  Picha za ultrasound zinaweza kutathmini ukubwa wa tezi dume na kutambua shida zingine kama kudhoofika kwa tezi,kupanuka kwa njia ya mkojo na kibofu au usaha.Picha hizi pia hutumika kutathmini kiwango cha mkojo unaobaki baada ya kukojoa. Ikiwa kiasi cha mkojo ni chini ya mililita hamsini,basi inaonyesha mkojo wa kutosha unatoka , mililita mia moja hadi mbili au zaidi huonyesha kuna kasoro na basi uchunguzi hufanywe.Kumbuka kipimo cha kidole nyuma na sonografia ni vipimo viwili muhimu kwa utambuzi wa kukua kwa tezi dume.
 • Kipimo cha nambari ya dalili
  (Prostate Symptoms Score or index)

  Kipimo hiki chenye chanzo chake Marekani huwezesha kutambua ugonjwa wa kibofu.Maswali yanayohusiana na ugonjwa huu huulizwa ili kutathmini matatizo yaliyopo. Hivyo kiasi cha shida iliyopo hujulikana kwa kuhesabu dalili zilizopo.

Kupima kwa kutumia kidole kwenye njia ya choo kubwa na sonografia ni vipimo viwili muhimu sana vya ugunduzi wa tezi dume lililovimba.

 • Uchunguzi wa maabarani
  Uchunguzi huu hauwezi kusaidia katika kutambua ugonjwa wa tezi dume,bali hutumika kutambua matatizo yanayohusiana nao.Mkojo hupimwa ili kutambua maambukizo,na damu hupimwa ili kutathimini uwezo wa figo.Kuna kipimo tofauti cha saratani ya tezi dume.
  Prostate Specific Antigen (PSA) hiki ni kipimo muhimu sana cha damu cha kuchunguza saratani ya tezi dume.
 • Uchunguzi zaidi-uchunguzi zaidi ili kutathmini kasi ya mtiririko wa mkojo, uvimbe na matatizo mengine ni pamoja na kuchukua kipande cha tezi dume, IVP,CT urogram,cystoscopynk

Je, mtu mwenye tezi dume iliyotanuka anaweza kuwa na saratani pia?

Ndio. Dalili za magonjwa haya mawili hufanana.Kwa hiyo vipimo vya kawaida vilivyotajwa haviwezi kutambua ugonjwa wa saratani.Lazima vipimo maalum vya saratani vifanywe. Vipimo hivi ni kumpima mgonjwa nyuma kwa kidole, kipimo cha damu kuona kiwango cha PSA nakuchukua kipande cha tezi dume (prostate biopsy).

Dalili za tezi kilichopanuka na saratani hufanana.Lazima uchunguzi wa kina ufanywe ili kujua ni ugonjwa upi mgonjwa anaugua kati ya haya mawili.

Matibabu ya tezi dume

Mambo yanayozingatiwa katika matibabu ya tezi dume ni pamoja na ukali wa dalili na jinsi shughuli za mgonjwa zinavyoathirika na dalili za ugonjwa huu. Lengo la matibabu huwa ni kupunguza makali ya dalili,kurahisisha maisha,kupunguza mkojo unaobaki kibofuni na pia kuzuia matatizo yanayokuja na ugonjwa huu.

Kuna njia tatu za matibabu:

A. Kubadilisha maisha na kungoja.
B. Matibabu ya dawa.
C. Upasuaji.

A. Kubadilisha maisha na kungoja

Hii ndiyo njia inayopendekezwa kwa wanaume ambao wana dalili kidogo ambazo haziwasumbui.Hata hivyo,haimaanishi kukaa tu bila kufanya chochote.Wakati mgonjwa anangoja,anahitajika kubadili jinsi anavyoishi ili kupunguza dalili zilizopo,na pia kumwona daktari kila mara(walao mara moja kwa mwaka) ili kujua kama dalili zinapungua au zinazidi.

 • Badili mazoea ya kukojoa na kutumia vinywaji.
 • Kojoa mara kwa mara,usizuie mkojo,kojoa mara tu haja ijapo.
 • Kojoa kwa vipindi viwili, yaani kwanza kojoa kama kawaida, ngoja kidogo na ujaribu kukojoa tena papohapo,usijilazimishe kukojoa.
 • Usinywe pombe wala kahawa jioni.Hivi viwili hulegeza kibofu na kufanya figo kitengeneze mkojo na hivyo basi kukojoa zaidi usiku.
 • Usinywe maji mengi sana.Usizidi lita tatu kwa siku.Usinywe maji mengi mara moja bali unywe kidogo kidogo siku nzima/mchana wote.
 • Punguza vinywaji unapoenda kulala au unapoenda kwenye shughuli nje.
 • Usinunue dawa za homa dukani.Hizi huzidisha dalili na mkojo kutotoka.
 • Badilisha wakati unapokunywa dawa za kukojoza.
 • Jichunge na baridi, weka mwili wako na joto na fanya mazoezi. Kutokufanya mazoezi huzidisha dalili.
Tezi dume lililovimba na ambalo linaleta dalili ndogo ndogo linaweza kuangaliwa kwa uangalifu na kwa kubadilisha mfumo wa maisha bila ya kuchukua hatua yoyote ya kidaktari.

 • Fanya mazoezi ya mifupa ya nyonga ili ipate nguvu. Mifupa hii ndiyo hushikilia kibofu na kusaidia kufunga njia ya mkojo.Mazoezi haya ni kukaza na kuachilia misuli ya nyonga.
 • Jaribu kukojoa baada ya muda fulani siku yote.
 • Pata matibabu unapofunga choo.
 • Punguza mfadhaiko.Kufadhaika na wasiwasi husababisha kukojoa zaidi.

B. Matibabu ya dawa
Dawa ndizo hutumika na hupendekezwa mara nyingi katika kukabiliana na dalili zenye ukali kiasi.Dawa hupunguza dalili kwa kiasi kikubwa kwa wagonjwa wengi.Kuna aina mbili za dawa, za kulegeza misuli ya kibofu,na za kupunguza ukubwa wa tezi dume.

 • Dawa za kulegeza misuli
  Hizi hulegeza misuli ndani na nje ya tezi dume, Hupunguza kizuizi cha mkojo na kuwezesha mkojo kutoka kwa urahisi zaidi. Dawa hizi zinaweza kusababisha kizunguzungu, kichwa kuuma na kuhisi uchovu.Dawa hizi ni kama famsulosin, alfuzosin,terazosin na doxazosin
 • Dawa za kupunguza tezi dume
  Hizi hupunguza ukubwa,kuongeza mkojo unaotoka na pia kupunguza dalili.Hazifanyi kazi haraka kama zile za kulegeza misuli.Nafuu hupatikana baada ya kuzitumia kwa kama miezi sita.Huwa bora kwa walio na dalili kali.Matatizo ya dawa hizi ni kukosa ashiki ya kufanya mapenzi na hata kupunguza nguvu ya uume.
 • Matibabu ya mseto
  Dawa aina zote mbili zilizotajwa hapo juu huwa ni bora zikitumiwa kwa pamoja.Huleta nafuu kwa kiasi kikubwa kuliko zikitumiwa moja moja.Njia hii ni bora kwa wanaume wenye dalili kali,tezi dume kubwa zaidi na ambao hawafaidiki na dawa za dozi kali ya kulegeza misuli.
Matibabu ya kawaida yanapendekezwa kwa tezi dume lililovimba kidogo au kiasi. Ni vema upasuaji ukaachwa ( avoided). 150. Okoa Figo Lako

C. Njia ya upasuaji
Njia hii hupendekezwa kwa watu wafuatao:

 • Dalili kali ambazo hazisikii dawa.
 • Mkojo kuziba ghafla.
 • Maambukizo ya njia ya mkojo ya mara kwa mara.
 • Damu kwenye mkojo.
 • Figo kushindwa kufanya kazi kwa sababu ya shida ya tezi dume.
 • Mawe ya kibofu pamoja na tezi dume iliyopanuka.
 • kuongezeka kwa mkojo unaobaki baada ya kukojoa.

Upasuaji umegawanyika katika aina mbili kukatwa au kuchomwa.

Njia za kukatwa

Kuna njia tatu hapa: Kipande cha tezi dume kukatwa, kupasuliwa na tezi dume kutolewa.

1. Kukatwa sehemu /kipande cha tezi dume

Hii ndiyo njia ambayo kwa kawaida hutumiwa na huwa nzuri kuliko dawa.Husaidia wagonjwa wengi, asilimia themanini na tano hadi tisiini. Husaidia kwa muda mrefu. Daktari hukata sehemu iliyoziba kwenye njia ya mkojo.Ngozi haikatwi wala kushonwa, lakini mgonjwa lazima alazwe hospitalini kwa operesheni hii.

Dalili kali za kuvimba kwa tezi dume, mkojo kufunga, maambukizi yanayojirudiarudia ya mfumo wa mkojo, na figo kushindwa/kufeli ni dalili zinazohashiria umuhimu wa upasuaji.

Kabla ya upasuaji

 • Ni vizuri kuhakikisha mgonjwa yu katika hali nzuri kimwili.
 • Mgonjwa asivute sigara ili kuzuia maambukizo ya kifua ambayo huchelewesha kupona.
 • Mgonjwa anashauriwa asiendelee kutumia dawa zinazofanya damu nyepesi kama vile aspirin,warfavin au clopidogrel.

Upasuaji

 • Huchukua kati ya dakika sitini hadi tisini.
 • Mgonjwa hudungwa sindano ya nusukaputi na hupatiwa dawa za kuzuia maambukizo.
 • Wakati wa upasuaji,kifaa maalumu (resectoscope) huingizwa kwenye njia ya mkojo kupitia kwenye uume.
 • Kifaa hiki huwa kina mwanga na kamera ya kupiga picha, waya ya kukata sehemu ya tezi na pia kuziba mishipa ya damu, na njia inayopeleka maji ya kusafisha kwenye kibofu.
 • Sehemu inayokatwa hutumwa kwenye maabara ili ichunguzwe iwapo ina chembe chembe za saratani.

Baada ya upasuaji

 • Mgonjwa hukaa hospitalini kwa siku mbili hadi tatu baada ya upasuaji.
 • Baada ya upasuaji katheta au tyubu kubwa huingizwa kwenye njia ya mkojo hadi kwenye kibofu.
 • Maji maalum husukumwa hadi kwenye kibofu na kutolewa kwa mfululizo kwa saa kumi na mbili hadi ishirini na nne.
 • Maji haya huwa ni ya kutoa damu au damu iliyoganda baada ya upasuaji.
 • Mkojo ukionekana safi bila damu yoyote, basi katheta hutolewa.
Njia ya matibabu inayofaa na inayopendwa ya tezi dume kubwa ni TURP.

 

Ushauri baada ya upasuaji

Mambo yafuatayo husaidia mgonjwa kupona haraka

 • Kunywa maji mengi kusafisha kibofu.
 • Zuia kwenda choo na hasa choo kigumu kwani huzidisha kutokwa na damu.Ukifunga choo tumia dawa ya kuharisha.
 • Usitumie dawa za kufanya damu kuwa nyepesi bila ushauri wa daktari.
 • Usifanye kazi ngumu kabla ya wiki nne hadi sita.
 • Usifanye kitendo cha ndoa kabla ya wiki nne hadi sita.
 • Usinywe pombe, kahawa wala vyakula vyenye viungo vikali.

Matatizo yanayoweza kujitokeza

 • Matatizo yanayoweza kutokea ni kutokwa na damu au maambukizo.Pia matatizo mengine ya kawaida yanayotokana na upasuaji.
 • Matatizo ya baadaye ni njia ya mkojo kuwa nyembamba, kukosa nguvu ya kufanya mapenzi au manii kurudi kwenye kibofu.
 • Hali hii ya manii ya mwanamme kurudi nyuna kwenye kibofu hutokea kwa wagonjwa wengi.Hutokea kwa takriban asilimia 70% ya wagonjwa. Lakini huwa haitatizi uwezo wa kufanya mapenzi lakini humfanya mwanamme gumba, yaani hawezi kuzaa.
 • Hali ambazo huenda zikasababisha matatizo zaidi ni kama vile uzito mkubwa, uvutaji wa sigara, pombe, kukosa lishe bora au ugonjwa wa kisukari.
TURP hufanywa kwa kupiga sindano mgongoni. Mgonjwa hapotezi fahamu na haitaji kukaa kwa muda mrefu hosipitalini.

Muone daktari iwapo:

 • Unashindwa kukojoa.
 • Maumivu makali ambayo hayatulizwi kwa dawa.
 • Kutokwa na damu yenye madonge makubwa iliyoganda, ambayo yanaweza kuziba katheta.
 • Dalili za maambukizo kama homa, baridi au kutetemeka.
 • Upasuaji wa kibofu ndiyo njia bora zaidi ya kutibu tezi kibofu kilichotanuka.
 • Upasuaji hufanywa kwa kutumia nusu kaputi iwekwayo mgongoni. Hii upunguza siku za kukaa hospitalini.
 • Manii/shahawa kuingia kwenye kibofu ni tatizo la upasuaji na kumfanya mgonjwa asizae.

2. Njia ya tezi kibofu kupasuliwa

Njia hii huwa nzuri kwa wanaume wenye tezi kibofu ndogo au afya upasuaji wa tezi dume kupitia njia ya mkojo (tupi).

Njia hii ni kama zile ambapo tezi inapunguzwa kwa kukatwa lakini badala ya sehemu kutolewa, mikato mirefu yenye kina hupasuliwa kwenye tezi dume.Mikato hii hupanua njia ya mkojo na kuwezesha mkojo kutoka kwa urahisi.

Faida za upasuaji huu ni pamoja na kupoteza damu kidogo, matatizo yanayo ambatana na upasuaji huwa kidogo, muda mfupi hospitalini na kupona haraka.Pia ile hatari ya mkojo au manii kurudi nyuma huwa nadra.Kasoro za njia hii ni kutofaulu katika kumaliza tatizo kabisa,na pengine tatizo kurudi tena.Wakati mwingi wagonjwa hurudia kutibiwa baadaye kwa ile njia ya kupunguza tezi dume kwa kukata sehemu yake. Upasuaji huu (TUIP) si njia mwafaka kwa wagonjwa wenye tezi dume kubwa.

TUIP ni njia mbadala ya TURP kwa wanaume wenye tezi dume dogo na ambao upasuaji wa TURP si mzuri kwao.

3. Upasuaji

Hapa mgonjwa hufunguliwa tumbo na tezi dume hutolewa.Siku hizi njia hii haitumiki sana kwa sababu kuna njia nyingine nyepesi ambazo zimegunduliwa.Njia hii hutumika tu kwa wazee ambao tezi zao zimekuwa kubwa sana au wenye matatizo mengine yanayohitaji upasuaji huu.

Njia zisizo za upasuaji

Njia hizi huwa hazina maumivu mengi kwa sababu ya uvumbuzi wa kitekenolojia. Njia hizi hulenga kutibu tatizo la tezi dume kwa kupanuka kwa njia rahisi iwezekanavyo:Njia hizi kwa kawaida hutumia joto,miale,na nguvu za umeme kupunguza tezi dume.Njia hizi zote hufanywa kwa kupitia njia ya mkojo ya yurethra iliyo kwenye uume. Faida za njia hizi nyepesi huwa ni :muda mfupi wa kukaa hospitalini,dawa kiasi ya ganzi (Anaesthesia),hatari na matatizo kidogo kuliko upasuaji na pia kupona haraka.

Kasoro zake ni pamoja na uwezekano wa ugonjwa kurudi baada ya muda fulani na hivyo mgonjwa kuhitaji upasuaji, mara nyingi baada ya miaka mitano hadi kumi.Kwa sababu sehemu ya tezi haitolewi,uchunguzi wa magonjwa mengine kama vile saratani haufanywi kwa hivyo usalama wake si kama ule wa sehemu ya tezi kutolewa.Shida nyingine ni kuwa njia hizi zisizo za upasuaji hazipatikani kwenye nchi zinazoendelea kwa urahisi na pia huwa ghali.Njia nyingine zisizo za upasuaji zinazotumika kutibu tezi dume iliyotanuka huwa ni;

 • Kuchoma kwa mawimbi ya sitima.
 • Kumomonyoa kwa sindano.
 • Kuchoma kwa maji moto.
 • Kuwekwa springi au koili.
 • Kuchomwa kwa miale.
Faida za MIT: Hatari ni chache na hulazwa kwa muda mfupi hosipitalini.

1. Kuchomwa kwa joto la wimbi la maikro : sehemu ya tezi iliyoziba njia ya mkojo huchomwa/huunguzwa.

2. Kumomonyoa kwa kutumia sindano ya umeme : kwa kutumia nguvu za umeme, sehemu ya tezi iliyoziba mtiririko wa mkojo hugadishwa na kuondolewa.

3. Kuchomwa kwa maji moto : Maji moto husababisha sehemu ya tezi ambayo haitakikani kuganda na kuondolewa.

4. Kuwekwa springi au koili : Springi au koili huwekwa katika sehemu ya yurethra iliyofinywa ndani ya tezi ili kuiweka wazi na kurahisisha mkojo kupita.

5. Kuchomwa kwa miale : sehemu iliyoziba njia ya mkojo humalizwa kwa kuchomwa.

Je,mgonjwa wa tezi dume lililotanuka anafaa kumwona tena daktari lini?

 • Akishindwa kukojoa kabisa.
 • Kuwashwa au uchungu akikojoa, mkojo wenye harufu mbaya, homa na kuhisi baridi.
 • Damu kwenye mkojo.
 • Kushindwa kuzuia mkojo na nguo za ndani kulowa mkojo.
Kuweka bangili ( stent)kwenye tezi dume ni matibabu salama na yanayofaa hasa wakati matibabu ya kawaida hayakufaa na upasuaji haupendekezwi.